Monday, 21 July 2008

EOTF: Ni kitendawili?

Nimesoma hii habari na kuona ni kweli inahitaji majibu, wengine mnasemaje?
...............................................................................


(SOURCE: Nipashe 2008-07-21 08:43:22 Na Simon Mhina)
Chama cha NCCR-Mageuzi, kimeitaka serikali kuutaifisha mara moja Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) unaomilikiwa na Mama Anna Mkapa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Ilala, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Oganaizesheni na Uchaguzi, Bw. Faustine Sungura alisema muundo wa mfuko huo na hati ya kuandikishwa, unaonyesha wazi ni mali ya mke wa Rais.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mfuko huo ulichangiwa na Watanzania wengi, mashirika na taasisi za ndani na nje, wakijua kwamba ni mali ya Ikulu, kwa vile upo chini ya mke wa Rais.

``Tunaitaka serikali kuutaifisha Mfuko wa Fursa Sawa, kwa vile uliandikishwa kwa jina la mke wa Rais na ulipewa nguvu na serikali pamoja na taasisi zote,`` alisema Bw. Sungura.

Mkurugenzi huyo alisema hatua ya Mama Mkapa kuendelea kuushikilia mfuko huo, kunatoa tafsiri kwamba, lengo la EOTF halikuwa kuwasaidia Watanzania.

Alisema utata uliojitokeza hivi karibuni kwamba Mama Mkapa ana hisa katika taasisi moja ya fedha, ni wazi kwamba mfuko huo umegeuzwa kampuni ya biashara na kwamba malengo ya kuanzishwa kwake sasa hayapo tena.

``Mfuko huu ambao umeanzishwa kwa jina la Ikulu, uliheshimiwa sana kwa sababu hiyo, lakini cha kushangaza umeporwa na mtu ambaye si mke wa Rais,``alisema.

Bw. Sungura alisema yeye asingekuwa na neno iwapo tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, ungejulikana kwa jina binafsi la Mama Mkapa lakini kamwe sio mke wa Rais.

Alisema iwapo serikali haitautaifisha mfuko wa EOTF, basi ipige marukufu wake za marais kuanzisha mifuko, kwa vile inatumika kama ndoano ya kuchotea fedha na kutumika kama chombo cha kifisadi.

``Sasa kama kila mke wa rais akija anaanzisha mfuko wake, tutakuwa na mifuko mingapi. Na kama kweli lengo lao ni kuwasaidia wanyonge, watoto na wanawake, kwa nini wasitumie mfuko mmoja kusaidia, kwa nini wasikae pamoja na kuuimarisha ili uwe mpana zaidi kuliko kuwa na vijimfuko vidogo vidogo vingi...Bila shaka hawataki utaratibu huo, kwa vile hii mifuko ni njia ya kuchotoa fedha,`` alisema.

Mathalani alisema, hivi sasa EOTF imekuwa mradi binafsi wa Mama Mkapa na hakuna mtu anayeweza kuhoji huku ukiwa umeanzishwa kwa jina la mke wa Rais, hatua ambayo alisema pia ni ufisadi.

``Kwa hiyo tunataka EOTF utaifishwe, unapoanzisha mfuko kama mke wa Rais, maana yake ni kwamba umeingiza jina la Rais katika mfuko, huo huwezi kukwepa. Na baada ya hapo serikali ipige marufuku wake za marais kuanzisha mifuko mingine, kwa kuwa kwanza kuwa mke wa Rais sio cheo,`` alisema.

Vile vile, Bw. Sungura alimtaka Mama Mkapa kutaja hadharani watu ambao wamechangia mfuko huo tangu uanzishwe, miradi ambayo mfuko huo unamiliki na makampuni ambao EOTF ina hisa.

Alisema iwapo Mama Mkapa atagoma kutangaza wafadhili wa mfuko wake, kama alivyogoma kumkabidhi Mama Salma Kikwete shughuli za EOTF, watathibitisha kwamba mfuko huo hakuundwa kwa nia ya kuwasaidia wanyonge.
.............................................................................

No comments: