Familia yagoma kumzika Wangwe
Maziko ya aliyekuwa Mbunge wa Tarime (CHADEMA), Bw. Chacha Wangwe, yameahirishwa baada ya kutokea mtafaruku kufuatia wazee na ndugu wa marehemu kutaka uchunguzi ufanyike baada ya kudai ndugu yao alipigwa risasi mdomoni iliyojitokeza kisogoni.
Kufuatia kuahirishwa kwa maziko hayo, mtafaruku mkubwa uliibuka baada ya kundi la vijana wa kijiji hicho waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, kuanza kurusha mawe hovyo na kusababisha wageni wakiwemo viongozi mbalimbali waliofika kwenye maziko hayo kukimbia.
Wazee wa kijiji cha Kemakorere waligoma mwili wa marehemu kuzikwa hadi hapo uchunguzi wa kina utakapofanywa upya na daktari kutoka Dar es Salaam na wao kuridhika na ripoti yake.
Kwa mujibu wa ratiba, maziko yalipangwa kufanyika jana saa 7.15 hadi saa 8 mchana lakini kuanzia asubuhi majira ya saa 3:00, ukoo wa Wangwe ulifanya mkutano chini ya mwenyekiti wake, Profesa Samwel Wangwe na kuazimia kuahirisha maziko hadi uchunguzi wa daktari kutoka Dar es Salaam utakapofanywa upya.
Habari zilisema mara baada ya mwili wa marehemu kufikishwa kijijini kwake Kemakorere, wanandugu na wazee waliutoa kwenye jeneza na kuuangalia ambapo baadhi ya wajumbe wa kikao hicho waligundua kwamba alipigwa risasi mdomoni iliyotokea kisogoni.
Baada ya kugundua hilo, wajumbe hao waliwaeleza waandishi wa habari kuhusu suala hilo, huku wakisisitiza maziko hayo yaahirishwe hadi uchunguzi wa kifo utakapofanywa tena.
Profesa Wangwe, ambaye ni kaka wa marehemu alisema baada ya ukoo kujadili kwa kina wameona kuwa kuna utata katika kifo hicho na kwamba hawataweza kuzika kama ilivyopangwa.
Alisema wameiomba serikali kuwa na subira hadi baada ya kuletwa daktari mwingine wa kufanya uchunguzi kwa madai kuwa hawana imani na uchunguzi uliofanywa awali.
Hata hivyo, ilipotimia saa 5 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Bw. Stanley Kolimba, ambaye alikuwa msimamizi wa mazishi hayo, aliiagiza kamati ya maandalizi ya madiwani kwenda kuutoa mwili wa marehemu Wangwe ili kuanza kwa ibada ambayo ingefanywa na Mchungaji wa Kanisa la Wasabato, Muso Stephen wa mtaa wa Nyabasi, lakini wana ndugu walikataa.
Viongozi wengi mashuhuri wa vyama na serikali na maelfu ya wananchi waliwasili kuhudhuria mazishi hayo.
Baadhi ya viongozi hao wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Ramadhan Feruzi, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Bw. Makongoro Nyerere, Mjumbe wa NEC, Christopher Gachuma, walilazimika kutimuka mbio baada ya tangazo la kuahirisha mazishi, kufuatia vijana kuanza kurusha mawe hovyo hali iliyoleta mtafaruku mkubwa.
Vijana hao walianza kukimbia huku wamebea mabango ambayo mengine yalikuwa yakiwa na ujumbe usemao, ‘bila Wangwe hakuna haki Tarime,` `viongozi mashuhuri kwa nini hufa kwa ajali na BP,` `tungeukagua mwili tungeridhika,` `Wangwe umekufa kweli kwa ajali au kwa risasi au kwa ushirikina,`.
Aidha, ndugu wa marehemu walilitaka Jeshi la Polisi kumweka chini ya ulinzi Deus Mallya, aliyekuwa ndani ya gari la marehemu wakati wa ajali iliyotokea Wilaya ya Kongwa, Dodoma, ili ahojiwe vizuri na kumtaja aliyempiga risasi Wangwe na siyo taarifa za kwamba marehemu alikufa kwa ajali.
Na katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, jana alinusurika kuuawa kwa mapanga baada ya kuwasili katika kijiji cha Kemakorere kuhudhuria mazishi ya marehemu Wangwe.
Hali hiyo ilianza kujitokeza saa 8:00 mchana baada ya Bw. Mbowe kuwasili kijijini hapo akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wengine wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Bw. Augustine Mrema (TLP), Bw. Joseph Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Bw. Bob Makani kiongozi mstaafu wa CHADEMA.
Baada ya kuwasili kwa viongozi hao, kundi kubwa la watu hasa vijana, walianza kumzonga Bw. Mbowe kwa kumuonyesha mabango mbalimbali ya kuonyesha kifo cha Wangwe si cha mapenzi ya Mwenyezi Mungu bali ameuawa.
Kufuatia hali hiyo, maofisa wa Usalama wa Taifa wakiongozwa na askari polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliwazuia wananchi hao kumzonga kiongozi huyo, lakini haikuwa kazi rahisi na hivyo kulazimika kumwingiza uani ambako shughuli za maandalizi ya mazishi hayo zilikuwa zikifanyika.
Hali hiyo ilifanya kubadilisha kabisa mazingira ya msiba huo, ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge na wanasiasa, viongozi wa wawakilishi kutoka nchini Kenya na maelfu ya wananchi.
Mazingira hayo ya kutisha huku wananchi hao wakiwa wamebeba mapanga, mikuki, sime na fimbo wengine wakiwa wameziweka hadharani na wengine wamezificha katika makoti na kujificha migombani, ilimfanya kiongozi wa ukoo huo, Profesa Samwel Wangwe, kuwaeleza baadhi ya viongozi msimamo wa ukoo kabla ya kutangazwa hadharani.
Baada ya maelezo hayo ambayo yalimhusisha pia Mkuu wa Mkoa, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Riberatus Barlrow, Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, Bw. Kabwe Zitto na viongozi wengine wa ukoo iliwabidi kuingia ndani kwa dakika 10 kufanya mjadala wa kuzika ama la.
Baada ya dakika hizo, viongozi hao walitoka nje ambapo Profesa Wangwe alipanda jukwaani na kuanza kutoa matangazo ambayo muda wote yalikuwa hayasikiki kutokana na kelele za waombolezaji wakidai hawamtaki Mbowe bali wanataka Mbunge wao.
Hata hivyo, Bw. Kabwe, alionekana kuwakonga wananchi hao kwa kusema maneno ya kumpamba marehemu kuwa ni kiongozi aliyependa kutetea wanyonge hasa wapiga kura wake hivyo kulazimika kunyamaza na kusikiliza kilichokuwa kikielezwa na msemaji huyo wa familia.
``Sisi kama ukoo baada ya kupokea mwili wa marehemu na kuufikisha hapa maneno mengi yamesemwa na ili kuondoa maneno hayo tumeona ni vizuri tukachunguza mwili wa marehemu kwa kutumia mtaalam wetu ambaye atawasili wakati wowote kuanzia sasa naomba sasa tuwe watulivu wakati tukisubiri hatua hiyo na mwili leo hauzikwi,`` alisema Profesa Wangwe huku akishangiliwa.
Kauli hiyo pamoja na kuonyesha imani kwa wananchi, lakini wengine walianza kutoa maneno yaliyomlenga Mbowe kuwa wanataka Mbunge wao sio Mbowe.
Hali hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Mara, kusimama na kuomba amani.
Hata hivyo, kauli hizo hazikueleweka kwa wananchi hao hasa vijana, hivyo kumlazimu mkuu huyo kuita polisi na kuanza kumsindikiza Mbowe katika gari lake ambapo pamoja na ulinzi huo mkali, lakini bado wananchi hao walimfuata hadi alipoingia ndani ya gari na kusindikizwa kwa ulinzi mkali kuelekea Tarime kisha Musoma.
Pamoja na Mbowe na viongozi wengine waliohudhuria msibani hapo wakiwemo hao wa Kenya, kila mmoja aliondoka kivyake na kuanza kuhaha kutafuta magari ya kuwavusha kuepuka kipigo hicho kilichokuwa kikitangazwa na wananchi.
Kiongozi wa wabunge 20 waliotumwa kuwakilisha Bunge, Bw. William Shelukindo, akielezea hali hiyo alisema katika historia hajawahi kuona kitendo kama hicho lakini imeonyesha jinsi wananchi hao walivyompenda Mbunge wao.
``Imesikitisha kweli imenifanya kutosoma salamu za Spika wa Bunge hata kutoa ubani wa Bunge tumekimbia kuepuka kufa pale...sasa vitu hivi vitaandaliwa utaratibu wake lakini nawaomba wananchi watulie wamzike mbunge wao,`` alisema Shelukindo.
Kwa upande wake waziri aliyewakilisha serikali, Bw. Steven Wassira alisema kitendo hicho kimewasikitisha lakini alisema hakuna njia ya kupata ukweli wa kifo cha mbunge huyo ni vema familia kama ilivyoamua kufanya uchunguzi huo upya katika kujiridhisha.
Awali baada ya Profesa Wangwe kutoa kauli hiyo Bw. Kabwe alisema uchunguzi watahakikisha unafanyika na kutangaza hadharani matokeo yake na kusema tayari polisi wamemkamata mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri na mbunge huyo siku ya ajali.
Shughuli za ujenzi wa kaburi hadi hatua hiyo inafikiwa ilikuwa imekamilika na hadi jioni hii hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuwa mwili wa marehemu huyo utazikwa lini.
(SOURCE: 2008-08-01 11:15:21
Na George John, PST Tarime, Nipashe)
...........................................................................
Friday, 1 August 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment